Thursday, February 18, 2016

Makampuni jitokezeni kujitangaza kupitia uwanja wa Taifa.

 Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akipata maelezo kuhusu michoro ya viwanja vya ndani vinavyotarajiwa kujengwa pembeni mwa uwanja wa taifa jijini Dar es salaam kutoka wa Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ( watatu kulshoto) na katibu Mkuu wake Profesa Elisante Ole Gabriel (wapili kushoto) wakati alipozungumza na wadau wa michezo kwenye uwanja wa Taifa leo Februari 17, 2016
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wadau wa michezo nchini kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam leo Februari 17, 2016.
 Baadhi ya wapenzi na viongozi wa michezo nchini wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza na wadau wa michezo nchini kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam leo Februari 17, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa michezo nchini baada ya kuzungumza ao kwenye uwanja wa taifa jijini dar es salaam leo Februari 17, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana  na wadau wa michezo nchini baada ya kuzungumza nao kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam Februari 17, 2016.

Na Lilian Lundo - Maelezo
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameyataka makampuni na wafanyabiashara kutangaza biashara zao kupitia uwanja wa Taifa.

Mhe. Majaliwa aliyasema hayo jana katika mkutano wa wadau wa michezo wakiwemo wadhamini wa michezo, vyama vya michezo vya Taifa na mashirikisho uliofanyika katika moja ya kumbi zilizopo uwanja wa Taifa.

“Uwanja wetu una hadhi ya kimataifa lakini uwanja huu hautumiki kutangaza biashara yoyote kama chanzo cha mapato, badala yake kuta za uwanja zimezungukwa na giza hasa muda cha usiku,” alisema Mhe. Majaliwa.

Mhe. Majaliwa aliongeza kwa kusema kuwa kama uwanja huo utazungukwa na mabango ya matangazo yataupandisha hadhi na kubadilisha mandhari ya uwanja hasa muda wa usiku na fedha zitakazopatikana zitatumika kuboresha uwanja huo.

Hivyo Mhe. Majaliwa amewataka wadhamini wa michezo kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo ya kutangaza bidhaa au huduma wanazozitoa kupitia uwanja wa Taifa ambao hutumika katika mechi nyingi za kitaifa na kimataifa zinazochezwa nchini.

Aidha, Mhe. Majaliwa amesema kuwa Tanzania itaendelea kupata heshima kupitia sekta ya michezo kwani michezo ni kielelezo kinachoweza kutambulisha utamaduni wa Taifa hivyo wadau wa michezo washikamane na Serikali na kuona ni namna gani matatizo ya michezo yatatatuliwa na michezo kuendelezwa nchini.

Serikali ya awamu ya tano imejipanga kuendeleza michezo nchini kwa kuweka misingi imara ya kuendeleza michezo kuanzia umri wa chini, kurekebisha sera na sheria za michezo ziliopitwa na wakati, kujali mafanikio, matatizo na mambo muhimu yanayohusu michezo.

No comments: