Thursday, February 18, 2016

UFAFANUZI KUHUSU TAKWIMU ZA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO.
UFAFANUZI KUHUSU TAKWIMU ZA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inayo miongozo inayosimamia ufuatiliaji wa magonjwa ya milipuko na miongozo hii imetolewa na kusambazwa katika mikoa na wilaya zote nchini. Mwongozo huu unafuata utaratibu wa mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa ujulikanao kama “Integrated Disease Surveillance and Response (IDSR)”

Katika mwongozo huu, taarifa za magonjwa ya milipuko kama Kipindupindu pindi yanapotokea hutolewa taarifa mara moja kwa kutumia Ainisho sanifu yaani “Standard case definition”. Aidha maainisho haya ya utambuzi wa ugonjwa yapo kwa ajili ya jamii (Community case definition) na katika ngazi ya kituo cha Afya (Health facility Case Definition).

Aidha utambuzi huu wa ainisho la awali, huzingatia dalili za ugonjwa ili mgonjwa aweze kupatiwa huduma wakati taratibu za vipimo zinapofanyika. Vipimo huchukuliwa kwa wagonjwa 10 wa awali wanaohisiwa kuwa na ugonjwa wa Kipindupindu, na iwapo mmoja wao akithibitika kuwa na vimelea vya ugonjwa basi uwepo wa mlipuko wa ugonjwa husika hutangazwa.

Aidha kutokana na utaratibu huu, ni wagonjwa wa mwanzo tu ndio watakaochukuliwa vipimo, na wengine watakaoendelea kujitokeza huwa wanachukuliwa kuwa wana ugonjwa kwa kuwa wana mahusiano na ushirikiano na wagonjwa waliokwisha thibitika “epidemiological link”

Vipimo vya maabara huchukuliwa tena kwa baadhi ya wagonjwa watakaoendelea kuugua ili kuweza kuangalia mwenendo wa ugonjwa husika na pia kupima usikivu wa Dawa (Antimicrobial Sensitivity Test).

Wizara inaendelea kusisitiza mambo manne muhimu, 
1. Utoaji wa taarifa ya wagonjwa wapya wa Kipindupindu huzingatia Ainisho Sanifu yaani Standard case Definition bila ya kuwepo uthibitisho wa ugonjwa kimaabara

2. Pindi ugonjwa ukisha thibitishwa kwa wagonjwa wa awali kumi (10) katika Mkoa/Wilaya/Halmashauri husika tayari mlipuko wa ugonjwa huu unathibitishwa na kutangazwa.

3. Uthibishwaji wa ugonjwa kimaabara unafanyika tu kwa baadhi ya wagonjwa ili kuweza kuangalia mwenendo wa ugonjwa na pia kupima usikivu wa Dawa (Antimicrobial Sensitivity Test)

4. Baadhi ya watu wenye ugonjwa wanaweza kupimwa na kuonekana kutokuwa na vimelea vya ugonjwa husika mfano kipindupindu. Zipo sababu nyingi zinazoweza kupelekea kipimo kutoonyesha uwepo wa vimelea hivyo mojawapo ikiwemo wagonjwa kuanza kutumia dawa kabla ya kufika katika vituo vyetu vya tiba.

Kwa mfano katika Mkoa wa Dar es salaam kwa siku kumi zilizopita kuanzia tarehe 7 hadi 16 Februari wagonjwa 16 wa kipindupindu (Temeke 12 na Ilala 4) ambao walikidhi vigezo vya ainisho sanifu na kupata matibabu katika kambi ya kipindupindu ya Temeke kwa wagonjwa wa Temeke na Hospitali ya Amana kwa wagonjwa wa Ilala na hivyo kulazimu kutolewa taarifa kwa mujibu wa muongozo.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
17 FEBRUARI 2016.

No comments: