Friday, February 19, 2016

TCU YAFUTA VYUO VISHIRIKI VYA MTAKATIFU JOSEPH.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania Prof Yunus Mgaya akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Kuhusu uamuzi wa Tume kufuta usajili wa vyuo vikuu vishiriki vya Mtakatifu Joseph tawi la Songea. 
Picha na Raymond Mushumbusi MAELEZO

Na Nyakongo Manyama MAELEZO
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefuta kibali kilichoanzisha vyuo vikuu viwili vishiriki vya Mtakatifu Joseph ambavyo ni Chuo Kikuu kishiriki cha Sayansi ya Kilimo na Teknolojia (SJUCAST) na Chuo Kikuu kishiriki cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (SJUIT) vilivyopo Songea.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za Tume hiyo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania,  Prof. Yunus Mgaya amesema kutokana na mapungufu yaliyobainishwa na Tume ambayo ni matatizo ya ubora wa elimu na ukiukwaji wa Sheria za uendeshaji wa Chuo Kikuu kama ulivyobainishwa na Sheria ya Vyuo Vikuu hii  imepelekea Tume kuchukua hatua ya kufuta usajili wa vyuo hivyo.

“ kutokana na yaliyobainishwa hapo awali tunapenda kutaarifu umma kwamba ,Tume imejiridhisha kuwa hivi vyuo vikuu vishiriki viwili havitoi elimu ya Chuo kikuu ya viwango stahiki na ukizingatia wanafunzi katika Vyuo hivi ndio waathirika wakubwa wa matatizo yaliyopo”Alisema Prof Mgaya.

“Napenda kufafanua kwamba Vyuo vikuu vishiriki tuliyovifutia usajili ni tawi la Songea na Vyuo vingine vishiriki vya Mtakatifu Joseph vilivyopo Dar es Salaam na Arusha vitaendelea kufanya kazi kama kawaida”Alisema Prof Mgaya.

Prof Yunus Mgaya amesema wanafunzi wote wanaosoma katika vyuo vishiriki vilivyofutwa usajili wanaarifiwa kuwa watahamishiwa kwenye vyuo vikuu vingine vinavyofundisha programu za masomo zinazofanana na masomo wanayosoma hivi sasa chini ya utaratibu uliopangwa.

Amevitaja vyuo ambavyo watapelekwa wanafunzi walipo katika vyuo vishiriki vilivyofutwa usajili kuwa ni Chuo Kikuu cha kilimo Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),Chuo Kikuu cha  Kikatoliki cha Mwenge(MWECAU) na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha(RUCU).

Amesisitiza kuwa orodha ya majina ya wanafunzi na vyuo watavyohamishiwa yatawekwa kwenye tovuti ya Tume hivi karibuni na wale wote wanaonufaika na Mikopo toka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, mikopo yao itahamishiwa katika vyuo watakavyokuwa wamehamishiwa.

Vyuo vikuu vyote chini vinakumbushwa kufata Sheria na kuzingatia utoaji wa elimu inayokidhi viwango vya ubora vinavyokubalika kitaifa na kimataifa, hivyo Tume haitasita kuchukua hatua stahiki kwa chuo kikuu chochote kitakachobainika kutoa elimu isiyokidhi viwango vya ubora kwa kisingizio cha aina yoyote.

No comments: