Thursday, February 18, 2016

NAIBU WAZIRI KALEMANI AMPA SIKU TANO MWEKEZAJI KUSHUGHULIKIA ULIPAJI FIDIA.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (katikati), akiongozwa na baadhi ya viongozi wa Machimbo ya Dhahabu ya Matinje yaliyopo katika Kijiji cha Matinje Kata ya Mwashiku wilayani Igunga. Naibu Waziri alitembelea Machimbo hayo hivi karibuni akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tabora.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Medard Kalemani (Mwenye Suti-katikati) akipokea maelezo kutoka kwa Meneja wa Machimbo ya Matinje yaliyopo Kata ya Mwashiku wilayani Igunga, Charles Nogu, wakati alipotembelea Machimbo hayo akiwa katika ziara ya kazi hivi karibuni. 
Naibu Waziri wa Nishati na Madini (katikati) akikagua machimbo ya Matinje yaliyopo Kata ya Mwashiku wilayani Igunga, alipotembelea Machimbo hayo hivi karibuni. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Mbunge wa Manonga, wilaya ya Igunga, Seif Gulamali. Wengine pichani ni baadhi ya viongozi wa Machimbo hayo, wataalamu kutoka Wizarani, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Na Veronica Simba - Nzega
SERIKALI imetoa siku tano kwa mwekezaji wa madini ambaye ni Kampuni ya NMDC Limited kutoka India, kushughulikia utaratibu wa kuwalipa fidia wananchi wa Kata ya Ntobo iliyopo wilayani Igunga, mkoa wa Tabora, walioachia ardhi yao kumpisha mwekezaji huyo.

Agizo hilo lilitolewa juzi, Februari 17 na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani, wilayani Nzega alipokutana na viongozi wa Kampuni hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tabora kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya wizara yake.

Akiwa wilayani Igunga, Naibu Waziri alipokea taarifa kuwa mwekezaji huyo alipewa leseni nne za uchimbaji madini wa kati mwaka 2012 lakini mpaka sasa hajaanza shughuli za uzalishaji kutokana na kutolipa fidia za maeneo ya wakazi wa eneo hilo.

Kutokana na taarifa hiyo, Naibu Waziri aliagiza kukutana na Mwekezaji huyo ambapo walikutana naye juzi akiwa wilayani Nzega akiendelea na ziara yake. 

Katika kikao hicho, ilibainika kuwa, kiasi cha shilingi za Tanzania bilioni 20.7 zinadaiwa kama fidia kwa wananchi waliopisha eneo husika.

Ilielezwa kuwa, ulipaji huo wa fidia umekwama kutokana na mwekezaji huyo kutotaka kulipa fidia yote kwa wakati mmoja bali anataka alipe fidia kidogo kwa kuanzia na eneo dogo kati ya lile analomiliki ambalo anadai ndilo atakaloanza kufanyia kazi.

Aidha, alidai kwamba atakuwa analipa fidia kwa eneo lililobaki kulingana na atakavyokuwa akilitumia.

Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna Msaidizi wa Madini wa Kanda ya Kati-Magharibi, Humphrey Mmbando alimweleza Naibu Waziri kuwa, wananchi wa eneo husika wanalalamika kuwa tangia eneo lao lichukuliwe na mwekezaji huyo, shughuli zao zilizokuwa zikifanyika katika eneo hilo zimesimama na hivyo wanahitaji kulipwa fidia stahiki.

Kamishna Mmbando aliongeza kuwa, kufuatia malalamiko ya wananchi, Ofisi yake ilimtaka mwekezaji huyo awe ametoa majibu ya namna atakavyoshughulikia madai ya wananchi ndani ya siku 10 ambayo ilikuwa ni juzi, Februari 17, wakati kikao hicho kikikaa.

Kutokana na maelezo hayo, Naibu Waziri alitoa siku tano zaidi kwa mwekezaji huyo ili ashughulikie mambo kadhaa katika kutatua mgogoro huo.

Ndani ya siku hizo tano, Naibu Waziri alimtaka mwekezaji huyo, atoe taarifa rasmi ya kimaandishi kwa Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati Magharibi kuwa anakusudia kufanya uzalishaji kwa kuanzia na eneo dogo ndani ya leseni yake.

Pia, alimtaka mwekezaji huyo kumwomba Mthaminishaji wa Serikali kufanya uthamini kwa kujikita katika eneo lile tu ambalo anakusudia kuanza kulifanyia kazi.

Vilevile, Naibu Waziri alimtaka mwekezaji huyo kuzungumza na wananchi husika ili wakubaliane kiasi cha fidia atakachotoa kwao kwa kuzuia shughuli zao za kujipatia kipato katika eneo hilo kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.

Mbali na maagizo hayo, Naibu Waziri alimtaka mwekezaji huyo awaruhusu wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji katika eneo ambalo atakuwa hajaanza kulifanyia kazi.

“Nimewapa siku tano zaidi, mfanyie kazi maagizo niliyoyatoa vinginevyo, tutachukua hatua nyingine stahiki za kisheria dhidi yenu.”

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kalemani ameagiza kufutwa kwa leseni zote za madini ambazo hazifanyiwi kazi na maeneo hayo kugawiwa kwa wachimbaji wadogowadogo ili wayafanyie kazi na kulipa mrabaha kwa Serikali.

“Kwa kuanzia, katika eneo hili, nimeagiza leseni za utafutaji wa madini za kampuni za Kilimanjaro Mine na Mabangu Resources ziandikiwe taarifa ya kufutwa na tutaendelea na maeneo mengine,” alisema.

Alisema kuwa kuna wawekezaji wengi ambao wamekuwa wakishikilia maeneo kwa muda mrefu pasipo kuyafanyia kazi na hivyo kuikosesha Serikali mapato yatokanayo na kodi, pia kuwakosesha wananchi maeneo ya kufanyia kazi.

Awali, Naibu Waziri alitembelea Machimbo ya Madini katika Kijiji cha Matinje B, Kata ya Mwashiku wilayani Nzega ambapo mbali na kumpongeza mmiliki wa machimbo hayo, Jason Shinyanga, kwa kulipa mrabaha wa Serikali, alimtaka kuboresha mazingira ya uchimbaji katika eneo hilo.

Meneo aliyoagizwa kuboresha ni pamoja na kujenga nyumba za kulala watumishi wake pamoja na vyoo bora. “Tunakupa taarifa ya siku 60 urekebishe dosari hiyo, usiporekebisha, tutasahau kama umelipa mrabaha au la,” alisisitiza Naibu Waziri.

Aidha, Naibu Waziri aliwashauri wananchi wanaojishughulisha na uchimbaji kuhakikisha wanapata ushauri wa kitaalamu kutoka ofisi za madini katika maeneo yao kabla hawajaanza shughuli hizo.

Pia, aliwataka kuhakikisha wanakuwa na leseni halali za kuendeshea shughuli hizo za uchimbaji ili pamoja na mambo mengine kuongeza thamani ya maeneo yao pindi wanapotaka kuyauza au kuingia ubia na wawekezaji wa kati na wakubwa.

No comments: