All Right Receved by MR.PENGO 2016

Thursday, November 19, 2015

Serikali yapiga marufuku uuzaji, ununuzi wa karafuu kwa ‘vikombe’ kuepusha wizi na ukataji mikarafuu.....

Na Ali Mohamed

Serikali imepiga marufuku uuzaji na ununuzi wa karafuu usio rasmi (vikombe) kuepusha wizi wa karafuu mashambani na ukataji wa mikarafuu unaofanywa na baadhi ya watu kutokana na kuzoeleka kwa biashara hiyo. 

Wakizungumza katika nyakati tofauti Wakuu wa Wilaya za Unguja na Pemba wamesema hakuna ruhusa kwa mtu yoyote kuuza au kununua karafuu mbichi au kavu na atakaebainika kujihusisha na biashara hiyo atashughulikiwa ipasavyo.

Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdalla alisema tatizo la ununuzi wa karafuu kwa vikombe, wizi na ukataji wa mikarafuu kwa lengo la kuiba karafuu lipo.

Alibainisha kuwa Serikali haiwezi kuvumilia makosa hayo kwa sababu wanaofanya uhalifu huo hawana imani na Serikali haina imani nao. Alifahamisha kuwa watakaokamatwa watachukuliwa hatua kwa misingi ya kisheria. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Haji Makungu Mgongo alisema  Serikali ya Wilaya yake kupitia kamati za Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa kushirikiana na Masheha wataendesha zoezi maalumu la kuwakamata watu wanaojihusisha na masuala hayo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Alisema karafuu ni zao la uchumi wa Taifa hivyo Serikali ya Wilaya yake haitokuwa tayari kuona baadhi ya watu wakihujumu kwa wizi hasa kukata mkarafuu kwa tamaa ya kupata maslahi ya muda mfupi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Mohamed Omar Hamad alisema wizi wa karafuu ambao pia hupelekea kukatwa matawi na mikarafuu midogo unawakatisha tamaa wakulima.

Nae Mkuu wa wilaya ya Wete ambae pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Hassan Khatib Hassan alisema ukataji wa mikarafuu ni uhalifu mkubwa ambapo tatizo hilo limewahi kuripotiwa ofisini kwake.

Alishauri kurejeshwa kwa utamaduni wa uchumaji karafuu kwa kambi ambapo Wakulima na Wafanyabiashara ni vyema wakajenga kambi katika maeneo wanayochuma karafuu, kufanya hivyo kutapunguza uhalifu unatokea katika mashamba yao.

Wakuu hao wa Wilaya na baadhi ya Masheha walilishauri Shirika la ZSTC kuanzishwa dawati maalumu la kufatilia kesi za uhalifu dhidi ya karafuu na mikarafuu zinazoripotiwa katika vituo vya Polisi.

Mapema akiwasilisha malalamiko hayo ya wakulima kuibiwa na kukatiwa mikarafuu yao kwa Wakuu hao wa Wilaya Mkurugenzi wa Mfuko wa Maedeleo ya Karafuu Ali Suleiman Mussa alisema matatizo hayo yanawaumiza sana Wakulima.

Alisema wizi wa karafuu na ukataji wa mikarafuu unachangiwa na baadhi ya watu wanaonunua karafuu  mbichi ambapo kisheria ni kosa kwa vile Shirika la   ZSTC ndio Taasisi pekee  iliyopewa  mamlaka ya kununua na kuuza karafuu. 

Alisema Shirika kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu umejipanga kufanya usajili wa wakulima wenye mashamba na wanaokodi karafuu ambapo watapewa vitambulisho maalumu vya kuwatambua. Alifahamisha kuwa utaratibu huo utazuia wizi wa karafuu kwa vile wezi hawatokuwa na nafasi ya kuuza karafuu ZSTC.

Akizungumzia suala la ubora wa karafuu, Mkurugenzi huyo amewaomba Wakuu hao wa Wilaya kwa kushirikiana na Masheha kupiga vita uwanikaji usiozingatia ubora, (uwanikaji kwenye barabara, sakafu na juu ya bati) na kuwataka Wakulima kuendelea kutumia majamvi kwa shughuli za uanikaji.

Katibu ambae pia ni Mwanasheria wa Shirika la ZSTC Ali Hilal Vuai aliwakumbusha Wakuu hao wa Wilaya na Masheha kuwa kukata mikarafuu kwa ajili ya kuiba karafuu ama kwa matumizi mengine  yoyote ni makosa kwa mujibu wa sheria namba 2 ya Maendeleo ya Karafuu ya mwaka 2014.

Alisema sheria hiyo inakataza  kuihujumu mikarafuu kwa aina yoyote ile na atakaebainika kufanya vitendo hivyo anapaswa kupelekwa katika vyombo vya sheria.

Aliwaomba Wakuu wa Wilaya kupitia Kamati zao za  ulinzi na usalama za Wilaya, Masheha na Polisi Jamii  kupambana na vitendo hivyo vya uhalifu dhidi ya biashara ya zao la karafuu vinavyofanywa na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu.
Post a Comment