Monday, June 15, 2015

TAIFA STARS YAANZAUSAJILI WA WACHEZAJI KUANZA JUNI 15 MWAKA HUU



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - RELEASE NO. 98
TAREHE 15 JUNI, 2015
TAIFA STARS YAFUNGWA NA MISRI
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, leo imepoteza mchezo wake wa kwanza kuwania kufuzu kwa fainali za AFCON mwaka 2017 baada ya kufungwa kwa mabao 3 - 0 na wenyeji Misri.

Taifa Stars ilicheza vizuri kipindi cha kwanza na hasa sehemu ya ulinzi ilifanya kazi ya ziada kuokoa mashambulizi ya washambuliaji wa timu ya Misri, na kupelekea kwenda mapumziko -0 - 0.

Kipindi cha pili Misri walifanya mabadiliko yaliyowapelekea kupata mabao hayo 3 ndani ya dakika 10, kupitia kwa Ramy Rabia(60), Basem Morsy(64) na Mohamed Salah (69). 

Stars ilifanya mabadiliko ya kuwaingiza Frank Domayo, Saimon Msuva na Salim Mbdonde na kufanya shambulizi kadhaa langoni kwa Misri lakini mashambulzi hayo yaliokolewa na walinzi wa timu ya Misri.

Mara baada ya mchezo huo, Taifa Stars inaondoka leo Alexandria kuelekea Cairo ambapo itaondoka na shirika la ndege la Ethiopia saa 8 usiku na kufika jijini Dar es salaam jumanne saa 7 mchana.

Tanzania: Deogratias Munish, Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Aggrey Morris/Salim Mbonde, Nadir Haroub, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto/Saimon Msuva, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samata, Amri Kiemba/Frank Domayo.

Misri: Ahmed El Shenawy, Ahmed Hegazy, Ramy Rabea, Mohamed Abd Elshafy, Hazem Emam, Mohamed Elneny, Ibrahim Salah, Mahmoud Abd Elmonem/Ramadan Soffiy, Mohamed Salah/Mostafa Ftahy, Doly Elgabay/Basem Morsy, Ahmed Hassan Meky.

USAJILI WA WACHEZAJI KUANZA JUNI 15
Usajili wa wachezaji kwa hatua ya kwanza msimu huu (2015/2016) unaanza Juni 15 hadi Agosti 6 mwaka huu wakati kipindi cha kutangaza wachezaji walioachwa au kusitishiwa mikataba ni kuanzia Juni 15-30 mwaka huu.

Kipindi cha kwanza cha uhamisho wa wachezaji ni kuanzia Juni 15 mwaka huu hadi Julai 30 mwaka huu. Kupitia majina na kutangaza pingamizi ni kati ya Agosti 7 na 14 mwaka huu. Kuthibitisha usajili hatua ya awali ni Agosti 15 hadi 19 mwaka huu.

Usajili hatua ya pili utakuwa kati ya Agosti 17 na Septemba 8 mwaka huu. Kupitia na kutangaza majina ya pingamizi hatua ya pili ya usajili ni kuanzia Septemba 8 hadi 14 mwaka huu. Uthibitisho wa usajili hatua ya pili ni Septemba 15 na 17 mwaka huu.

Wachezaji wanaotoka nje ya Tanzania, usajili wa mtandao wa FIFA wa TMS utakuwa wazi kuanzia kesho (Juni 15) hadi Septemba 6 mwaka huu. Klabu zinazosajili wachezaji kutoka nje zinatakiwa kufanya hivyo kupitia akaunti zao za mtandao wa TMS.

Kwa klabu ambazo hazina akaunti ya TMS zinatakiwa kuwasiliana na TFF ili mameneja wao wa usajili wapatiwe mafunzo ya TMS, na baadaye kuombewa akaunti hizo FIFA.

Kwa upande wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inatarajiwa kuanza Agosti 22 mwaka huu, na ratiba inatarajiwa kutoka mwezi mmoja kabla (Julai 22 mwaka huu). 

Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inatarajiwa kuanza Septemba 12 mwaka huu, wakati Ligi Daraja la Pili (SDL) inatarajia kuanza Oktoba 17 mwaka huu.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: