Sunday, April 12, 2015

WATANZANIA WAISHIO NJE KUTOPIGA KURA OKTOBA - PINDA.



WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Watanzania waishio ughaibuni hawataweza kupiga kura wakiwa nje ya nchi kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu, kwa sababu kuna mambo kadhaa ambayo Serikali inabidi iyatekeleze kabla ya zoezi hilo kufanyika.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Aprili 11, 2015) wakati akizungumza na baadhi ya Watanzania waishio Uingereza kwenye makazi ya UBalozi wa Tanzania nchini humo, Balozi Peter Kallaghe, yaliyoko Highgate, Kaskazini mwa Jiji la London.

Akizungumza na Watanzania hao ambao baadhi yao walitoka miji ya Leicester na Manchester, Waziri Mkuu alisema mambo makuu ambayo yanahitaji kuzingatiwa kabla hawajaweza kupiga kura ni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 1985 pamoja na uandikishwaji wa Watanzania wana-Diaspora kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

"Najua suala kubwa ambalo mnatamani kulisikia ni hili la Watanzania kuweza kupiga kura kutokea huku mliko. Hili inawezekana lisifanikiwe wakati huu kwa sababu kuna mambo muhimu ya kuzingatia kubwa likiwa ni marekebisho ya sheria na hili zoezi la uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura. Ili mwananchi aweze kupiga kura ni lazima awe ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura," alisema.

"Itabidi tuangalie kama mashine za BVR nazo zitapaswa kupelekwa kwenye kila ubalozi ili watu wetu waweze kujiandikisha au itafutwe njia nyingine ya kufanikisha hilo jambo.... lakini watu wa Tume wanaamini kwamba jambo hilo linaweza kufanikiwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2020," aliongeza.

Waziri Mkuu ambaye aliwapatia nakala zisizopungua 40 za Katiba Inayopendekezwa, alitumia fursa hiyo kuwasisitizia wasome kwa makini Katiba hiyo ili wawe na uelewa mpana na kisha wailinganishe na Katiba ya mwaka 1977 ambayo inatumika hivi sasa ili waweze kubaini kama kweli haina kitu kama ambavyo watu wengine wanadai.

"Moja ya changamoto zinazotukabili huko nyumbani ni mjadala kuhusu Katiba Inayopendekezwa,wako watu wanaosema kwamba hakuna kitu kipya kabisa kwenye Katiba Inayopendekezwa, lakini mimi nasema hayo ni mawazo yao binafsi," alisema.

Akifafanua kuhusu Katiba hiyo, Waziri Mkuu alisema: "Mimi nilikuwa sehemu ya Bunge Maalum la Katiba, ni kweli tulibadili baadhi ya vipengele lakini kwa nia ya kuiboresha. Ninawasihi kila mmoja wenu aisome na kuangalia kama kweli hamna kitu au kuna kitu kipya ikilinganishwa na Katiba inayotumika hivi sasa. Angalieni na pimeni, je kuna kitu kimeboreshwa au la?"

Aliwasihi waendelee kuiombea nchi ya Tanzania ili iendelee kuwa na amani na utulivu na hasa katika kipindi hiki ambacho inakabiliwa na uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais. "Ninawasihi muendelee kuiombea nchi yetu ili ipate viongozi wazuri ambao watajali maslahi ya wengi," aliongeza.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, APRILI 12, 2015.

No comments: