Wednesday, January 14, 2015

MNUNUZI WA NYUMBA/KIWANJA USILAZIMISHWE KULIPA ASILIMIA KUMI SERIKALI ZA MITAA HAIPO KISHERIA.


Na Bashir Yakub
Mara nyingi nimekuwa nikiandika kuhusu masuala muhimu kuhusu ardhi hasa  namna ya kuandika mikataba  mtu anapokuwa ananunua nyumba/kiwanja , hadhi ya mikataba hiyo kisheria, na ubora wake. 
Pia nimeandika mambo mbalmbali kuhusu namna ya kununua nyumba au kiwanja kwa usalama ili watu wasitapeliwe. Nikasema suala si tu kununua kile unachokipenda na kuondoka isipokuwa ni kununua  na  kuwa salama  na ulichonunua  bila hatari ya kukumbana na mgogoro mbeleni. 
Lengo la haya yote ni katika kuhakikisha watu hawatapeliwi na hivyo kupoteza  fedha walizochuma kwa jasho.Lengo lingine ni kuwaepusha wanunuzi  na hatari ya kuingia mahakamani ambako kuna  usumbufu mkubwa na panapoteza fedha na muda sana tena sana, naongea hili kwa uzoefu. 
Leo pia nasisitiza tena kuwa  ili ununue kiwanja au nyumba  na uepuke kabisa kupata mgogoro hakikisha  unafuata taratibu zote za msingi na za kisheria   ikiwemo kuhakikisha  unaandaa mkataba wenye hadhi  ambao  hata likitokea tatizo basi mkataba uwe ndio mlinzi wako.  Aidha leo naongelea tatizo lingine tena katika  masuala hayahaya ya  manunuzi ya viwanja na nyumba. Naongelea fedha ambayo serikali za mitaa wamekuwa wakiichukua kutoka kwa watu wanaouziana  ardhi.

( 1 )  SERIKALI   ZA   MITAA   KUCHUKUA  ASILIMIA  KUM I  WAKATI   WA  MANUNUZI  YA KIWANJA/NYUMBA
Hatua hii  ya serikali  za mitaa  kuchukua fedha kutoka  kwa wanaouziana viwanja  au nyumba  limekuwa la kawaida sana. Kitu hiki kipo muda mrefu sasa lakini hakuna anayekemea au hata kusema.
Watu wanauziana kiwanja au nyumba  serikali za mitaa wanawaambia kuwa   mnatakiwa kulipa asilimia kumi kama ada ya mauziano .Asilimia kumi  ni hela  nyingi sana kwakuwa kama nyumba imeuzwa milioni mianne  asilimia kumi ni  sawa na milioni arobaini.  
Zipo serikali za mitaa nyingine ambazo wakati mwingine hudai  chini ya hizo lakini mara kwa mara   asilimia kumi ndio huwa inaombwa. Kinachouma zaidi hawa jamaa wa serikali za mitaa huwa wanalazimisha  kutolewa kwa fedha hizo. Hufikia hadi hatua ya kutoa vitisho na ikitokea kuwa mtu ameuza bila kuwa taarifu ili wachukue hela  basi wanamjengea uadui  na hata yule aliyenunua naye anajengewa uadui.

( 2 ) ASILIMIA   KUMI   YA  SERIKALI  ZA  MITAA  HAIPO   KISHERIA.
Ni  jambo la kushangaza  sana. Hakuna sheria yoyote katika nchi hii ambayo inatambua asilimia kumi. Hili ni jambo la kuzuka tu  na limeanzishwa kwa matamanio(tamaa)  ya watu. 
Narudia tena hakuna katika sheria yoyote ya nchi hii inayosema kuwa watu wanapouziana kiwanja au nymba  inatakiwa  muuzaji au mnunuzi alipe asilimia kumi serikali za mitaa.Asilimia kumi  ni mradi wa watu tu ambao wamekubaliana ili kujipatia kipato. 
Ni mradi ambao  umeanzishwa kwa muda sasa na umekuwa ukirithishwa kizazi hadi kizazi. Natoa  changamoto( challenge) ukimuona kiongozi yoyote wa serikali za mitaa kwa nia njema tu muulize  asilimia kumi wanayotoza au gharama yoyote ile wanayotoza wakati wa mauzo  ya viwanja na nyumba  inapatikana katika sheria ipi. Namba yangu ya simu iko chini hapa akikupatia sheria hiyo nijulishe. Kwa uhakika hatopata kitu kama hicho kwa kuwa ni kitu ambacho  hakipo.
( 3 ) KAMA  ASILIMIA  KUMI  HAIPOI  KISHERIA  BASI  NININI ?.
Jibu ni rahisi  kuwa asilimia kumi au malipo yoyote unayoyatoa  serikali za mitaa wakati wa ununuzi wa nyumba/kiwanja  ni rushwa. Ni rushwa na ni ufisadi.  Ifahamike wazi kuwa viongozi wa serikali za mitaa ni watumishi  wa serikali. Fedha yoyote ambayo hulipwa serikalini ni lazima iwe imeainishwa  katika sheria fulani. 
Hakuna malipo yoyote kwa serikali ambayo hutolewa bila ya kuwa  yameainishwa pahala fulani. Pili fedha  yoyote halali inayolipwa kihalali katika mamlaka  yoyote ya serikali  ni lazima itolewe risiti ya serikali. Inatolewa risiti ya serikali  ikiwa na maana kuwa inatambuliwa na serikali , itakwenda serikalini  na matumizi yake yatakaguliwa na serikali.  Fedha yoyote inayotolewa kwa serikali bila aliyetoa kupewa risiti ni fedha ambayo ina ufisadi ndani yake. 
Na katika maana hiyo ni kuwa unapolipa fedha serikali  za mitaa kwasababu yoyote ile  kuhusu kufanyika kwa mkataba wa manunuzi ya kiwanja/nyumba  unakuwa umetoa rushwa ndugu na  kama utachukuliwa hatua utatakiwa kujibu mashtaka ya kutoa rushwa. Kutoa rushwa nako ni kosa si kupokea tu ndio kosa. 
Kiongozi wa serikali za mitaa anayeomba na kupokea fedha hizo  anakuwa ameomba na kupokea rushwa.  Na ndio maana fedha hizi hazitolewi  risiti. Kama kuna mtu aliwahi kunua ardhi na akalipa fedha serikali za mitaa na akapewa risiti atanipigia simu aniambie. Hakika hakuna  na kama ulipewa ilikuwa ya kuzuga tu kwa kuwa hakuna risiti ya malipo hayo. 

( 4 ) UNAPONUNUA   KIWANJA/NYUMBA   SI LAZIMA   KUWASHIRIKISHA  SERIKALI   ZA MITAA.
Kisheria unaponunua kiwanja au nyumba pahala fulani suala la  kuwashirikisha serikali za mitaa ni hiyari yako. Mtu asikulazimishe eti ni lazima serikali za mitaa wawepo. Na hata wakiwepo uzito wao kama itatokea mgogoro  ni sawa na uzito wa shahidi mwingine yoyote ambaye ungeenda naye katika mauziano. 
Mahakamani serikali za mitaa ni shahidi sawa na shahidi ambaye si kiongozi wa serikali za mitaa kama itatokea mgogoro. Ieleweke kuwa wanaouziana wanao uhuru kisheria kabisa kuwashirikisha serikali za mitaa au kutowashirikisha. Serikali za mitaa hulazimisha kuingia katika manunuzi  ili wapate chao.
Basi wanunuzi mjue kuwa kutowashirikisha serikali za mitaa katika kununua  haiondoi uhalali wa ulichonunua na wala haikipunguzii hadhi hata chembe kisheria ulichonunua.Hapa naongelea sheria na hivi ndivyo ilivyo.Wasikulazimishe  kuwashirikisha au  kutoa hela.   

MWANDISHI  WA  MAKALA  HAYA  NI MWANASHERIA  NA  MSHAURI WA SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI  LA  HABARI  LEO  KILA JUMANNE, GAZETI JAMHURI  JUMANNE, NA  GAZETI NIPASHE  JUMATANO.
0784482959
0714047241
                                                 bashiryakub@ymail.com

No comments: