Saturday, January 10, 2015

MHE. CHIKU GALLAWA AMEFANYA ZIARA YA UKAGUZI KWENYE MACHINJIO YA KISASA KIZOTA MKOANI DODOMA.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Chiku Gallawa akikagua utunzaji wa nyama kwenye chumba maalumu cha kutunzia nyama zinazosubiri kusafirishwa kwenye machinjio ya Kisasa Kizota Mjini Dodoma Januari 9, 2015.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Chiku Gallawa akifanya majumuisho ya ziara yake ya ukaguzi kwenye machinjio ya Kisasa Kizota Mjini Dodoma Januari 9, 2015, wengine ni wafanyakazi wa machinjio hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Chiku Gallawa akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa machinjio ya Kisasa Kizota mara baada ya kufanya ziara ya ukaguzi kwenye machinjio hayo Januari 9, 2015.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Chiku Gallawa ameiagiza Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya, Manispaa ya Dodoma na wadau wa maendeleo ya sekta ya Mifugo kukomesha mara moja tabia ya uchinjaji wa mifugo kiholela nje ya Machinjio ya Kisasa ya Kizota iliyopo Mjini Dodoma.
Alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki (Jan 9,2015) alipofanya ziara ya ukaguzi kwenye Machinjio hiyo ya kisasa iliyopo Kizota Mjini Dodoma inayomilikiwa na kuedeshwa kwa ubia kati ya serikali (NARCO) na kampuni ya National Investment Company Limited (NICOL) ambapo kwa pamoja wameunda kampuni ya Tanzania Meat Company (TMC).
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa alibaini sekta hiyo ya uchinjaji katika Manispaa ya Dodoma inakabiliwa na tatizo kubwa la uchinjaji kiholela nje ya Machinjio hiyo iliyopewa jukumu la uchinjaji mifugo (Ngombe, Mbuzi, Kondoo) kisheria ndani ya Manispaa ya Dodoma jambo ambalo ni hatari sana kwa usalama wa afya za walaji na kukosesha serikali mapato.
Katika kuendesha vita hiyo ya kukomesha tabia ya uchinjaji mifugo kiholela katika Manispaa ya Dodoma, Mhe. Gallawa amewataka wataalamu wa mifugo wa Mkoa na Manispaa ya Dodoma kwa kushirikiana na Kampuni ya TMC kuendesha mazoezi ya ukaguzi kwenye maeneo yote yanayohusishwa na uchinjaji holela na kuwachukula hatua wote watakao bainika kufanya hivyo kwa kuwa wanapingana na sheria za Afya na Mazingira.
Mhe. Gallawa ametaka mazoezi hayo ya ukaguzi kuwa endelevu na kuhusisha hadi ngazi za msingi za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye Manispaa ya Dodoma na kuagiza awe anapewa mrejesho kila mara ukaguzi huo utakavyokuwa ukifanyika.
Taarifa iliyotolewa na uongozi wa Machinjio inaeleza kuwa moja ya changamoto kubwa zinazokabili sekta ya uchinjaji mifugo katika Manispaa ya Dodoma ni uchinjaji kiholela nje ya Machinjio hiyo ya kisasa iliyoko Kizota ambayo ndio imepewa jukumu kisheria la kuchinja katika Manispaa ya Dodoma.
Taarifa hiyo inaongeza kuwa  mara nyingine mifugo hususan Ngombe wanaochinjwa kiholela hua wagonjwa ama Ng’ombe wa wizi na hua wanachinjiwa maporini, mafichoni, minadani ama wengine wanakwepa ushuru. Vilevile taratibu za uchinjaji zinakuwa za kienyeji haziendani na kanuni za Afya na Mazingira na wakati mwingi hakuna ukaguzi wa madaktari wa mifugo kuthibitisha kama nyama zinafaa kwa matumizi ya binadamu/Kuliwa lakini cha kushangaza nyama hizo zinauzwa maeneo mbalimbali ya mji wa Dodoma.
Taarifa ya uongozi wa Machinjio ilimaliza kwa kusema changamoto nyingine ni upatikanaji wa mfugo bora kwa ajili ya kuchinja machinjioni hapo kwani kwa sasa soko na mahitaji yake ni makubwa sana kutoka nchi za kiarabu kama Oman, Dubai, Quwait na nchi ya China na hata ndani ya nchi.
Mwanzoni mwaka 2004 machinjio ilianza kwa kuchinja Mbuzi 200 na Ng’ombe 50 kwa siku lakini kwa mwaka 2014 ilipanda kufikia mbuzi 1200 na Ng’ombe 150 kwa siku na malengo ya mwaka huu 2015 ni kufikia mbuzi 2000 na ngombe 300 kwa siku na kuwa ngombe wote hao ni kwa ajili ya matumizi ya ndani pekee isipokuwa mbuzi wengi ni kwa ajili ya usafirishaji.

No comments: