Saturday, January 10, 2015

MAALIM SEIF AFUNGUA ICU HOSPITALI YA MNAZI MMOJA,ZANZIBAR.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad na Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bw. Xie Yun Liang, wakifurahi baada ya kukata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU), katika hospitali ya Mnazi Mmoja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akitembelea wodi mpya ya wagonjwa mahututi (ICU), katika hospitali ya Mnazi Mmoja, baada ya kuifungua rasmi.
Baadhi ya wanafunzi wa chuo cha afya Mbweni, wakiwa sehemu ya washiriki katika hafla ya ufunguzi wa wodi ya wagonjwa mahututi katika hospitali ya Mnazi mmoja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU), katika hospitali ya Mnazi Mmoja.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr. Mohamed Saleh Jidawi, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU), katika hospitali ya Mnazi Mmoja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akigana na Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bw. Xie Yun Liang, baada ya kumalizika hafla ya ufunguzi wa kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU), katika hospitali ya Mnazi Mmoja. Wa pili kulia ni Waziri wa Afya Mhe. Rashid Seif Suleiman. (Picha na Salmin Said, OMKR)

Na: Hassan Hamad, OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewasisitiza wananchi kufuata taratibu na maelekezo ya hospitali, ili kuwawekea wagonjwa mazingira bora.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika hafla ya ufunguzi wa kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) cha hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 51 na Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema wagonjwa hasa wanaotibiwa katika wodi ya wagonjwa mahututi wanahitaji utulivu na uangalizi maalum, hivyo hakuna budi kwa wananchi kwa watendaji wa hospitali na wananchi kuwawekea mazingira bora kwa ajili ya matibabu yao.
Amesema iwapo wananchi watashindwa kufuata taratibu hizo ambazo zimewekwa kwa lengo la kuweka mazingira bora ya hospitali, wanaweza kusababisha usumbufu na athari zisizokuwa za ulazima kwa wagonjwa, ikiwa ni pamoja na kuwasababishia matatizo mengine ya kiafya.
Sambamba na hilo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amewahimiza wafanyakazi wa hospitali kuwa wapole na wavumilivu wakati wote, ili kuwapa matumaini wagonjwa na wananchi wanaofika hospitali kwa ajili ya kupatiwa huduma.
Amesema kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu kwa wafanyakazi wa hospitali kutokuwa na lugha nzuri wakati wanapowahudumia wagonjwa, jambo ambalo linakiuka maadili ya taaluma ya afya.
Amesema wakati umefika kwa wafanyakazi hao kubadilika ili kulinda heshima ya taaluma hiyo na kujenga matumaini mapya kwa wagonjwa wanaofika hospitali.
“Kitendo cha kumjali mgonjwa ikiwa ni pamoja na kumpa lugha nzuri ni sehemu ya matibabu kwa mgonjwa huyo, na hapo hapo anaweza kujisikia kuwa amepata nafuu kutokana mapokezi mazuri aliyoyapata. Kwa hivyo watendaji wa afya mnatakiwa kuwa na nyuso za tabasamu wakati wote mnapowahudumia wagonjwa”, alitanabahisha Maalim Seif.
Maalim Seif amewatahadharisha watendaji wa sekta ya afya kuacha kuhatarisha maisha ya watu kwa sababu ya kushindwa kuchangia gharama za matibabu.
Amesema kitu cha msingi ni kuweka mazingira ya kujaribu kuokoa maisha ya mgonjwa kwanza, na gharama za matibabu zinaweza kujadiliwa baada ya mgonjwa kupata nafuu.
Hata hivyo Maalim Seif ameelezea kuridhishwa kwake na hali nzuri ya wodi hiyo mpya ya wagonjwa mahututi, na kuelezea matumaini yake kuwa itatunzwa na kuendelezwa.
Amesema kuwepo kwa wodi hiyo yenye vitendea kazi vya kisasa katika hospitali ya mnazi mmoja, kutasaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa waliokuwa wakisafirishwa nje ya Zanzibar kutafuta huduma hiyo.
Aidha Maalim Seif ameitaka Wizara ya Afya kuweka mkazo katika utoaji wa mafunzo na kuwaendeleza vijana katika taaluma ya afya, ili kupunguza tatizo la wataalamu wa sekta hiyo.
Mapema akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Afya Mhe. Rashid Seif Suleiman, amesema serikali inajitahidi kupata vifaa vya kisasa vya uchunguzi, ili kuwawezesha madaktari kufanya kazi zao kwa uhakika.
Amesema katika kuimarisha sekta ya afya, Wizara hiyo ina mpango wa kupata dawa kwa ajili ya matumizi ya Zanzibar bila ya kupita muda wake wa matumizi, sambamba na kujenga wodi mpya ya akinamama wanaokwenda kujifungua katika hospitali hiyo.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dr. Mohamed Saleh Jidawi, amesema lengo la kujengwa kwa wodi hiyo mpya ni pamoja na kuinua afya za wananchi pamoja na kuokoa maisha yao.
Amefahamisha kuwa wodi hiyo sasa imeimarika kwa kuwa na vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya uchunguzi na upimaji, na kwamba hatua hiyo itaondosha tatizo la wagonjwa hao kupelekwa sehemu nyengine kwa uchunguzi.
Wodi hiyo yenye vitanda vinane na vifaa vya uchunguzi, imetengenezwa kwa mashirikiano katika Serikali ya China na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na imegharimu dola milioni moja nukta mbili hadi kukamilika kwake.

No comments: