Friday, March 4, 2016

MALALAMIKO YANAYOHUSU UPATIKANAJI WA HAKI KUSHUGHULIKIWA KWA WAKATI.

 Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Katiba na Sheria  Bi Farida Khalfan (katikati) akizungumza na waandishi wa habari(Hawapo Pichani) kuhusu utaratibu wa Wizara katika kupokea na kushughulikia malalamiko yanayohusu upatikanaji wa haki kwa wananchi. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya malalamiko  Grifin Mwakapeje na kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Ufatiliaji Haki Bi Mary Mrutu.
 Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya malalamiko kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Grifin Mwakapeje akitoa rai kwa wananchi na wadau wa sekta ya Sheria kuendelea kutumia huduma ambazo zinazotolewa na Wizara hiyo ili kuwezesha kupata haki kwa wakati. 
                Mkurugenzi Msaidizi Ufatiliaji Haki Bi Mary Mrutu kutoka Wizara ya Katiba akifafanua kwa waandishi wa habari (Hawapo Pichani) mamlaka ya Waziri wa Katiba na Sheria katika kuongeza muda wa ukomo wa kufungua mashauri ya madai mahakamani.

Na Frank Mvungi-Maelezo.
SERIKALI imedhamiria kuendelea kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi yanayowasilishwa ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wakati.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Malalamiko kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Griffin Mwakapeje wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

aAidha , Mwakapeje amesema Wizara hiyo imekuwa ikipokea malalamiko yanayohusu ucheleweshwaji wa utekelezaji wa amri mbali mbali zinazotolewa na mahakama,ucheleweshaji wa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri baada ya kumalizika mahakamani.
Malalamiko mengine yanahusu msongamano wa mahabusu, ucheleweshwaji wa upelelezi,wananchi kubambikiwa kesi,migogoro ya ardhi navitendo vya rushwa.

Akizungumzia wajibu wa  Wizara hiyo Mwakapeje amesema ni kuyaratibu na kuyawasilisha kwenye taasisi husika ili kupata muafaka wa malalamiko hayo kwa wakati.

Hatua nyingine inayochukuliwa na Wizara katika kuwasaidia wananchi kupata haki kwa wakati, ni kutoa msaada wa kisheria unapohitajika kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo ili kuwawezesha wananchi kupata haki kwa wakati.
Katika kushughulikia malalamiko hayo “Serikali inayo dhamira ya dhati yakuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki kwa wakati.” Amesema Mwakapeje.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara hiyo Bi Farida Khalfan akizungumzia Mfumo wa kupokea malalamiko amesema kuwa wananchi wanaweza kufika katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo mtaa wa Sokoine au kuandika barua ili kuwasilisha malalamiko yao na yatafanyiwa kazi kwa wakati.

Wizara ya Katiba na Sheria ina Dhamana ya Kusimamia masuala ya Katiba na Sheria ambapo inatoa huduma mbali mbali za kisheria kwa wananchi,mashirika na taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

No comments: