Friday, February 26, 2016

SERIKALI YAWAKUTANISHA VIJANA KUUNDA KANUNI ZA UENDESHAJI BARAZA LA VIJANA TAIFA.

 Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye ulemavu Bw. Eric Shitindi akizungumza na vijana (hawapo pichani) alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa maendeleo ya vijana katika kuchangia uandaaji wa kanuni za uendeshaji wa Baraza la Vijana Taifa jana jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa maendeleo ya vijana katika kuchangia uandaaji wa kanuni za uendeshaji wa Baraza la Vijana Taifa jana jijini Dar es Salaam.
 Mwezeshaji Bw. Patrick Kipangula (aliyesimama) akitoa mada kwa wadau wa maendeleo ya vijana wakati wa kikao cha kuchangia uandaaji wa kanuni za uendeshaji wa Baraza la Vijana Taifa jana jijini Dar es Salaam.
 Mjumbe  wa maendeleo ya vijana akichangia mada wakati wa kikao cha kuchangia uandaaji wa kanuni za uendeshaji wa Baraza la Vijana Taifa jana jijini Dar es Salaam.
 Wawakilishi kutoka Mamlaka mbalimbali za Serikali, Asasi za kiraia, Vyama vya siasa, Taasisi za kidini, Vijana wenye ulemavu, Shule za sekondari na Shule za msingi wakifuatilia kwa makini mada zilizokua zikiendelea wakati wa kikao cha kuchangia uandaaji wa kanuni za uendeshaji wa Baraza la Vijana Taifa jana jijini Dar es Salaam.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye ulemavu Bw. Eric Shitindi (watatu kushoto waliokaa) katika picha ya pamoja na vijana wenye ulemavu wakati wa kikao cha kuchangia uandaaji wa kanuni za uendeshaji wa Baraza la Vijana Taifa jana jijini Dar es Salaam. Wapili kulia (waliokaa) ni Mkurugenzi Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi, wapili kushoto ni Mwenyekiti wa kikao Bw. Godwin Kunambi, na wanne kulia (waliosimama) ni Mkurugenzi msaidizi Vijana Bibi. Ester Riwa
Picha na: Genofeva Matemu - Maelezo

Na; Genofeva Matemu – Maelezo
SERIKALI imedhamiria kuhakikisha kuwa vijana wanakuwa na chombo chao chenye kujali utaifa, uzalendo na maslai bila kujali itikadi za kisiasa, kidini, rangi, hali za kiuchumi, jinsia na maumbile kwa kuandaa kanuni zitakazolifanya Baraza la Vijana Taifa kuwa huru na lenye haki.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu Bw. Eric Shitindi alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa maendeleeo ya vijana katika kuchangia uandaaji wa kanuni za uendeshaji wa Baraza la Vijana Taifa jana jijini Dar es Salaam.

“Nimuhimu kuunda Baraza kisheria litakalokuwa na uwakilishi wa vijana wa makundi yote ili liweze kutumika katika kuleta umoja na mshikamano wa kitaifa” alisema Bw. Shitindi
Aidha Bw. Shitindi amelipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kutunga sheria Na. 12 ya mwaka 2015 ya Baraza la Vijana Taifa ambalo litaleta maendeleo ya vijana na nchi kwa ujumla.

Akizungumza katika kikao hicho mwenyekiti aliyeteuliwa kuongoza mjadala huo Bw. Godwin Kunambi amesema kuwa Vijana takribani 120 wamepata fursa adhimu ya kushiriki katika uandaaji wa kanuni za uendeshaji wa Baraza la Vijana Taifa hivyo kuwataka vijana hao kujadili mambo ya msingi yatakayowawezesha wananchi wa Tanzania hususani vijana kutatua kero zao kupitia Baraza hilo.

Naye mwakilishi kutoka kundi la watu wenye ulemavu Bw. Gaston Hemed Mcheka ameipongeza Serikali kutoa nafasi kwa kundi la watu wenye ulemavu kuwa na uwakilishi kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa pindi Baraza la Vijana Taifa litakapoanza ambapo kundi hilo litatumia nafasi hiyo kutatua changamoto zinazowakabili.

Kikao cha wadau wa maendeleo ya vijana katika kuchangia uandaaji wa kanuni za uendeshaji wa Baraza la Vijana Taifa kimeshirikisha takribani vijana 120 kutoka Mamlaka mbalimbali za Serikali, Asasi za kiraia, Vyama vya siasa vilivyosajiliwa, Taasisi  za kidini, Vijana wenye ulemavu, Shule za Sekondari pamoja na Shule za msingi.

No comments: