Wednesday, May 20, 2015

SHERIA MPYA YA TAKWIMU KUONGEZA UFANISI WA SHUGHULI ZA KITAFITI NA UPATIKANAJI WA TAKWIMU SAHIHI NCHINI.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu ujio wa sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015 iliyopitishwa na Bunge Mwezi Machi mwaka huu leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi hiyo Bw. Morrice Oyuke.
Wadau mbalimbali na waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati akitoa ufafanuzi kuhusu ujio wa sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015.

Na. Veronica Kazimoto.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa Sheria Mpya ya Takwimu ya mwaka 2015 haina lengo la kuzuia Taasisi au watu binafsi kufanya tafiti zao hapa nchini bali inalenga kuweka misingi imara ya shughuli za kitakwimu na tafiti zenye ulinganifu unaotokana na mfumo rasmi  utakaoondoa uwepo wa takwimu zinazokinzana. 

 Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu ujio wa sheria hiyo mpya iliyoridhiwa na Bunge Mwezi Machi mwaka huu.

Amesema kuanzishwa kwa sheria hiyo kunalenga kutoa mwongozo kwa Taasisi za Serikali na Mashirika mbalimbali yanayozalisha takwimu hapa nchini ili yaweze kuendesha shughuli za ukusanyaji na usambazaji wa takwimu kwa kuzingatia sheria hiyo mpya na kuwa huru kutoa takwimu sahihi  zinazoendana na uhalisia wa Tanzania. 

“Sheria hii hailengi kuondoa uhuru wa taasisi nyingine za tafiti kufanya kazi zao, taasisi zote za utafiti zinazotambulika kisheria zitaendelea kuwa huru katika kufanya tafiti kwa mujibu wa taratibu zao ilimradi tu zinafuata sheria hii” Amesisitiza Dkt.Chuwa.

Amefafanua kuwa kifungu cha 20 cha sheria hiyo kinaeleza kuwa takwimu zinazotolewa na taasisi nje ya Serikali kwa kukidhi vigezo vya kitakwimu vilivyowekwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ikiwemo uzingatiaji wa mbinu za kukokotoa takwimu zitatambuliwa kuwa rasmi na zitatumika katika kupanga mipango ya maendeleo ya nchi.

 Dkt. Chuwa amebainisha kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu wanaofanya tafiti ambazo wanasimamiwa na wahadhiri wa vyuo vikuu ipo sheria inayowalinda na kusimamia matokeo ya tafiti hizo ambazo husambazwa kwa utaratibu uliowekwa kwa sheria zilizoanzisha vyuo vikuu.

Aidha ,kuhusu  makosa yaliyoanishwa katika  sheria hiyo mpya ya takwimu ambayo adhabu yake  imeainishwa katika kifungu cha 37 (3) ni kifungo kisichopungua miezi 6 au faini isiyopungua shilingi milioni moja.

Makosa hayo ni pamoja upotoshaji wa ukweli kuhusu takwimu rasmi utakaofanywa na vyombo vya habari, vitendo vya kuzuia msimamizi, mdadisi au karani wa Sensa kutekeleza majukumu yake kisheria,kukataa kwa makusudi kujaza fomu au nyaraka yoyote au kujibu maswali yaliyoulizwa, kutoa taarifa zisizo sahihi, kuharibu fomu au nyaraka yoyote na  mtu yeyote kujifanya msimamizi , mdadisi au karani wa Sensa kwa lengo la kupata taarifa ambazo hastahili kuzipata.

Makosa mengine ni yale ya kushawishi mtu yeyote asishiriki katika zoezi la Kitakwimu linaloendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa mujibu wa sheria hiyo, kukataa kutoa nyaraka zozote zinazohitajika katika shughuli za kitakwimu na kukiuka kifungu chochote cha sheria hiyo.

Kuhusu mchakato wa kupatikana kwa sheria hiyo Dkt. Chuwa amesema umezingatia vigezo vyote ikiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa 19 kupitishwa muswaada wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, kujadiliwa  Bungeni, Muswaada huo kuwasilishwa kwa wadau ambao waliujadili na kutoa maoni ambayo yalisaidia kuboresha muswaada huo.

Pia amesema kutakuwa na kamati maalumu ya kitaalam itakayoundwa kwa ajili ya kuangalia takwimu zitakazokuwa zinakusanywa itakayofanya kazi zake kwa weledi ili kuhakikisha kuwa hakuna ukiritimba wowote unaojitokeza katika kuthibitisha na kupitisha tafiti na takwimu zitakazowasilishwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu. 

Pia amesema kutakuwa na kamati maalumu ya kitaalam itakayoundwa kwa ajili ya kuangalia takwimu zitakazokuwa zinakusanywa itakayofanya kazi zake kwa weledi ili kuhakikisha kuwa hakuna ukiritimba wowote unaojitokeza katika kuthibitisha na kupitisha tafiti na takwimu zitakazowasilishwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu.


Amesisitiza kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaendelea kutoa elimu kwa umma ikiwemo kuzumgumza na vyombo vya habari ili kujenga uelewa wa umuhimu wa sheria hiyo kwa maendeleo ya Taifa.

No comments: