Thursday, February 26, 2015

MWIJAGE AZITAKA KAMPUNI ZA MAFUTA KUBORESHA MAHUSIANO.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage (Kulia) akielekeza jambo kwa baadhi ya Viongozi wa Kampuni ya Mafuta ya TIPPER alipotembelea Kampuni hiyo hivi karibuni wakati wa ziara yake kwa Kampuni mbalimbali zinazojishughulisha na biashara ya mafuta nchini.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage (Wa pili kutoka Kushoto) akifuatana na baadhi ya Viongozi wa Kampuni ya Mafuta ya GAPCO kukagua miundombinu ya kuhifadhia mafuta iliyoko eneo la Kampuni hiyo, Kurasini jijini Dar es Salaam. Naibu Waziri alitembelea Kampuni mbalimbali zinazojishughulisha na biashara ya mafuta nchini kufanya mazungumzo na kukagua miundombinu inayotumiwa na Kampuni husika.
Meneja wa Kampuni ya Mafuta ya HASS nchini Tanzania, Ali Hassan Ahmed (Kushoto), akisikiliza maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage (aliyeinua mkono) kuhusu utekelezaji wa mambo mbalimbali unaotakiwa kufanywa na Kampuni hiyo, hususan kujenga mahusiano mema na jamii. Wa kwanza Kulia ni Mbunge wa Temeke (Viti Maalum – CCM), Mariam Kisaka.
Joshua Mtunda (mwenye Fulana ya Njano), akizungumza na Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage (wa Tatu kutoka Kushoto), kwa niaba ya Vijana wenzake wanaofanya biashara ya kusafirisha abiria kwa Pikipiki/Bodaboda kuhusu msaada wanaohitaji ili kuboresha biashara yao. Vijana hao wanafanya biashara yao eneo la Kigamboni karibu na ilipo Kampuni ya Mafuta ya HASS.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage (wa kwanza – Kushoto), akikagua miundombinu ya kuhifadhia mafuta ya Kampuni ya Mafuta ya PUMA katika eneo la Kampuni hiyo, Kurasini jijini Dar es Salaam. Pamoja naye pichani ni baadhi ya Viongozi wa Kampuni hiyo na Maafisa wa Serikali wanaoshughulikia Sekta ya Mafuta.

Na Veronica Simba

Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage amezitaka Kampuni zinazojishughulisha na biashara ya Mafuta nchini, kutumia mbinu mbalimbali za kuboresha mahusiano mema na jamii zinazowazunguka ili kujenga imani kwa wananchi na hivyo kupata ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulinzi wa miundombinu husika.

Aliyasema hayo katika ziara yake hivi karibuni alipotembelea Kampuni mbalimbali za Mafuta zilizoko jijini Dar es Salaam pamoja na kukagua miundombinu yao.

Mwijage alisema, matatizo kama vile kuharibiwa kwa miundombinu ya kuhifadhia na kusafirishia mafuta, pamoja na wizi wa mafuta unaofanywa na baadhi ya wananchi unachangiwa na wananchi kutokuwa na imani na wafanyabiashara hao kwa kuwa hawaoni manufaa ya moja kwa moja kwa jamii kutoka Kampuni hizo.

“Ikiwa wananchi wataona manufaa ya uwepo wa Kampuni zenu katika maeneo yao, nina uhakika watajenga imani kwenu na hawatakuwa tayari kuona mnaharibikiwa kwa namna yoyote kwani wao pia watakuwa ni sehemu yenu,” alisema Mwijage.

Akifafanua kuhusu namna nzuri ya kujenga mahusiano mema na jamii, Mwijage alisema inafaa Kampuni hizo ziwasaidie wananchi kuinua vipato vyao kwa kuwapatia mitaji ya fedha na vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya biashara mbalimbali.

Naibu Waziri alitoa mfano wa biashara ndogondogo za kusafirisha abiria kwa kutumia Pikipiki maarufu kama Bodaboda zinazofanywa na vijana, pamoja na biashara ya kuuza chakula maarufu kama Mama Lishe kwa akina mama na mabinti.

“Pamoja na mambo mengine makubwa mnayosaidia jamii kama vile kuchangia elimu, nashauri pia muone namna ya kusaidia mambo madogo madogo kama kuwanunulia bodaboda vijana pamoja na kuwapa mitaji akina mama lishe,” alisisitiza Mwijage.

Aidha, Mwijage alisisitiza Kampuni hizo kuwashirikisha Viongozi mbalimbali wa maeneo husika wakiwamo Wabunge, Madiwani, Viongozi wa Kata na Mitaa husika katika zoezi la kuainisha watu wanaohitaji misaada husika ili kuepuka utapeli kwa kuwapatia wasio na sifa zinazostahili kupata misaada hiyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri aliagiza Barabara ya Mafuta iliyoko eneo la Mivinjeni-Kurasini jijini Dar es Salaam ifunguliwe ili kupunguza msongamano wa magari unaochangia magari makubwa yanayosafirisha mafuta kwenda sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi kutokusafiri kwa wakati hivyo kusababisha hasara kwa Kampuni husika.

“Ninaomba Halmashauri ya Manispaa ya Temeke iangalie uwezekano wa kuifungua njia hii ambayo wameifunga, ili itumike kama ilivyokuwa ikitumika awali; magari yaingie na kutoka kwa urahisi ili kuepusha msongamano uliopo,” alisisitiza Mwijage.

Naibu Waziri alilazimika kutoa agizo hilo kufuatia hali ya msongamano mkubwa wa magari aliojionea kwa baadhi ya Kampuni alizotembelea ikiwemo Kampuni ya GAPCO iliyoko eneo la Kurasini.

Kwa upande wao, wawakilishi wa Kampuni zilizotembelewa na Naibu Waziri, waliahidi kuzingatia ushauri uliotolewa katika kuboresha mahusiano yao kwa jamii husika.

No comments: