Mbunge wa
viti maalum mkoa wa Mbeya, Dkt. Mary Mwanjelwa(CCM), amekabidhi madawati 84
katika shule za Msingi Itiji na Ivumwe zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la
Mbeya.
Akikabidhi
madawati hayo yenye thamani ya Shilingi Milioni tano jana, Katibu wa Mbunge
huyo, Tumaini Mwakatika, alisema kuwa, Mbunge alipokea mahitaji ya shule hizo
kutoka kwa viongozi wa maeneo ya shule, ndipo akaamua kuomba msaada huo kwa
wahisani ambao ni Benki ya NMB.
Alisema,
maombi ya viongozi hao yalikuwa mengi, lakini akaona ni vema akaanza na suala
la madawati linalogusa moja kwa moja taaluma na Afya za wanafunzi.
“Mbunge
anawashukuru NMB, lakini pia ametoa wito wa kutunza vema madawati hayo, na anawaombeni
wanafunzi kuzingatia masomo na kwamba wazazi waache ushabiki wa kisiasa na vyama
katika mambo ya maendeleo”Alisema Tumaini katika hotuba zake wakati wa
kukabidhi madawati 42 shule ya Msingi Itiji na 42 shule ya Msingi Ivumwe Jijini
Mbeya.
Meneja biashara
za Serikali kanda ya Nyanda za juu kusini wa benki hiyo ya NMB, Focus Lubende,
alisema kuwa, benki yake iliamua kutoa msaada huo baada ya kupata maombi kutoka
kwa Mbunge Dkt.mary Mwanjelwa.
“Baada ya
kupata maombi, tukafanyia kazi. Na katika mkoa wa Mbeya ni shule mbli tu
zimebahatika kupata msaada huu wa madawati ambazo ni Ivumwe na Itiji”alisema
Lubende.
Mwalimu mkuu
wa shule ya Msingi Itiji, Thomas Mwilenga, alishukuru kwa msaada huo wa
madawati 42 kwa shule yake, huku akiahidi kuitisha mkutano wa wazazi na
kuwaonesha madawati hayo yaliyotolewa na Mbunge kwa hisani ya benki ya NMB.
Diwani wa
viti maalum kata ya Mwakibete, Agness Mangasila, alisema amefarijika baada ya
kupata msaada wa madawati 42 kwa ajili ya shule ya Ivumwe, maana yeye ndiye alipeleka
maombi hayo kwa Mbunge Dkt. Mwanjelwa, baada ya kupata changamoto kutoka kwa
uongozi wa shule hiyo.
Mkuu wa
shule hiyo ya Ivumwe, Nestora Mbwanji, mbali na kushukuru, alisema shule yake
inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 18 ambapo kwa sasa vipo 10,
matundu ya vyoo vya wanafunzi wavulana 18, wasichana matundu 24 na wanafunzi
awali matundu manne.
“Tunashukuru
wa madawati haya maana tulikuwa na upungufu wa madawati 72 na sasa tumepata 42,
tuna upungufu wa vyumba vya madarasa na sasa kuna maboma matano yanayotakiwa
kumaliziwa kwasababu mlundikano wa wanafunzi darasani unaathiri taaluma ingawa
tumeendelea kushika nafasi za shule kumi bora katika mitihani ya Taifa” alisema
Mwalimu Mbwanji.
Alipoulizwa
idadi ya wanafunzi wa darasa la saba waliopo kwa mwaka huu na kulundikana
katika chumba kimoja cha darasa, alisema kuwa wanafunzi wanaotarajia kuhitimu
mwaka huu na wapo katika chumba kimoja ni 143.
Dkt. Mwanjelwa alisema huo ni utekelezaji wa ilani ya cham chake na ni wajibu kwa kiongozi kutafuta wafadhili kwa kuandika michanganuo ya miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Mwenyekiti
wa kamati ya shule ya Ivumwe, Zawadi Ndassoni, alisema tangu kuanzishwa kwa
shule hiyo mwaka 1976, madawati hayo ndiyo msaada mkubwa kuwahi kutolewa
shuleni hapo, ambapo alibainisha kuwa, Mbunge huyo ameandika historia katika
shule hiyo.
No comments:
Post a Comment