Wednesday, March 2, 2016

WAZIRI WA AFYA UMMY MWALIMU APOKEA MSAADA WA FEDHA WA MIL 220 KWA MATIBABUYA WAGONJWA WA MOYO

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Ally Mwalimu leo Machi 2.2016, amepokea msaada wa fedha kwa ajili ya kuwezesha matibabu ya wagonjwa wa moyo katika taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo kwa msaada huo, jumla ya watoto 101, wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo katika taasisi hiyo kwa gharama za fedha hizo zilizotolewa na Jumuiya ya Kihindu waishio Dar es Salaam ijulikanayo kama BAPS Charity, kwa kuguswa kwao na kutoa msaada mkubwa na upendo waliouonyesha kwa watanzania wanaosumbuliwa na maradhi ya moyo.

Wiziri Ummy amebainisha kuwa, kiasi cha msaada unaotolewa utawezesha wagonjwa wapato hao kupatiwa matibabu ya moyo hivyo kuwa, faraja kubwa kwa wagonjwa waliokuwa wakisubiria huduma hizo kwa muda mrefu kutokana na kushindwa gharama za matibabu yake.

Aidha, kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amepongeza kwa msaada huo kwani utasaidia kutoa matibabu kwa watoto hao 101, huku pia taaisi yake ikikabiliwa na changamoto ya wagonjwa wengi ambapo amezitaka taasisi na wadau wengine kujitokeza kuchangia ilikupunguza wagonjwa wanaosubiria kupatiwa matibabu hasa upasuaji.

Prof. Janabi ameeleza kuwa, matibabu ya wagonjwa wa moyo yana gharama kubwa kwani kwa mtoto mmoja ndani ya nchi yanafikia hadi Milioni nne (Mil 4) huku kwa nje ya nchi matibabu hayo yakifikia hadi Milioni 16, gharama hizo ni kubwa hivyo wadau na taasisi binafsi zimeombwa kujitokeza ilikuokoa maisha ya wagonjwa wengi hasa watoto ambao wapo katika taasisi hiyo na mikoa mingine.
Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi akisoma taarifa fupi juu ya magonjwa wagonjwa wa moyo wanaopatiwa matibabu katika taasisi hiyo na namna walivyojipanga kutoa matibabu ya upasuaji kwa watoto hao 101, waliolipiwa gharama za matibabu kutoka BAPS Charity. Wengine ni Waziri wa Afya, Mh. Ummy Mwalimu pamoja na viongozi wa BAPS Charity.
Waziri Ummy Mwalimu akiongea na mmoja wa wazazi waliokuwa katika tukio hilo la kukabidhiwa fedha kiasi cha Mil 220, kwa ajili ya wagonjwa wa moyo 101, ambao wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika taasisi ya JKCI.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akipata kumjulia hali mtoto Zahara Seleman Muna (10) ambaye anasumbuliwa na magonjwa ya moyo. Hata hivyo Waziri Ummy Mwalimu amejitolea kama Waziri kuhakikisha atawasaidia watoto hao katika kutimiza ndoto zao ikiwemo kuwasomesha na masuala mengine kupitia Wizara yake ambayo yenye dhamana, Waziri Ummy aliguswa na watoto hao kutokana na ndoto zao walizokuwa nazo ikiwemo kusoma zaidi.
Mwenyekiti wa taasisi ya BAPS Charity, Subhash Patel, akizungumza machache kuhusiana na mchango huo wa Milioni 220, kwa ajili ya matibabu ya watoto 101, ambapo pia aliomba wadau wengine kujitokeza kuchangia ilikuisaidia Serikali katika kuhakikisha uhai kwa wagonjwa wa moyo hasa watoto hapa nchini.
Bw. Alfred D. Dafi mkazi wa Karatu akiwa amembeba mtoto wake, Beatrice Alfred (13) akitoa shukrani zake kwa Waziri wa Afya, Mh. Ummy Mwalimu kwa kuweza kuchukua majukumu ya kumsaidia mtoto wake katika masuala ya kumsomesha na mambo mengine kama Waziri mwenye dhamana. Waziri amechukua jukumu ya kuwasaidia watoto hao, kutokana na kuguswa na ndoto walizonazo ikiwemo kusoma wafike mbali. Mtoto huyo Beatrice hadi sasa anasoma darasa la sita, katika shule ya Sumawe, iliyopo Karatu.
Dk. Naiz Majani, ambaye ni daktari wa watoto wa magonjwa ya moyo akitoa ufafanuzi kwa wanahabari juu ya matatizo ya magonjwa ya moyoo ambapo amebainisha kuwa kati ya asilimia 10, pekee magonjwa ya moyo yanabainika kwa mwanamke huku miongoni mwa wazazi wanaozaa watoto wenye matatizo ya moyo ni wale waliokosa chanjo mbalimbali ikiwemo ya Lubela na mambo mengine.
Watoto Beatrice Alfred (13) na Zahara Seleman Muna (10) wakiwa katika picha ya pamoja. Waziri wa Afya, Mh. Ummy Mwalimu ameamua kujitolea kuwasaidia kutimiza ndoto zao ikiwemo suala la kuwasomesha na mahitaji mengine kama Waziri mwenye dhamana. Kushoto ni Baba wa mtoto Beatrice, Bw. Alfred Dafi ambaye anatokea Karatu.Waziri Ummy Mwalimu akimpa pole dada wa Zahara Seleman Muna (10), Editha Foi,(kulia) aliyekuwa akilia kwa uchungu baada ya Waziri Ummy Mwalimu kuamua kujitolea kuwasaidia watoto hao iliwatimize ndoto yao ya elimu na mahitaji mengine kama Waziri Mwenye dhamana."Uchungu wa Mama", Waziri Ummy Mwalimu akiwa na watoto Beatrice na Zahara ambao wanasumbuliwa na magonjwa ya moyo, ambapo baada ya kuwajulia hali na kuguswa na ndoto zao za kielimu, Waziri Ummy Mwalimu ameguswa na watoto hao na kuamua kuwasaidia katika elimu na mambo mengine kama Waziri mwenye dhamana..Waziri Ummy Mwalimu akiwa akipeana mkono na kushikiria hundi ya sh. Mil 220, iliyotolewa na taasisi ya BAPS Charity kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto 101, wa magonjwa ya moyo waliopo katika taasisi ya JKCI. (Picha zote na Andrew Chale,Modewjiblog/MO tv)
.

No comments: