All Right Receved by MR.PENGO 2016

Wednesday, May 20, 2015

WAFUGAJI WALIOVAMIA ENEO LA LOLIONDO WATAKIWA KUONDOA MIFUGO YAO.

  Waziri  wa Maliasili  na  Utalii  Lazaro  Nyalandu  (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania, Mbarouk Nassor Mbarouk (wa tatu kulia), wengine ni wawakilishi kutoka balozi huo. (Picha  zote na Loveness  Bernard)
Waziri  wa Maliasili  na  Utalii  Lazaro  Nyalandu  akiwa  amebeba  ndoo  ya maji  kichwani  alipokuwa  akikabidhiwa  visima  33 vilivyochimbwa kwa msaada  wa Watu  wa Falme  za Kiarabu  na Balozi  wa Falme  hizo.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akifungua bomba la maji kuashiria uzinduzi wa mradi mkubwa wa maji katika Kata ya Olosokwani, Loliondo wilayani Ngorongoro, juzi. Mradi huo umefadhiliwa na Serikali ya Falme za Kiarabu (UAE) ambayo imewekeza wilayani humo. Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na Balozi wa UAE nchini Tanzania, Mbarouk Nassor Mbarouk.
 WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akijindaa kumtwisha ndoo ya maji mkazi wa Kata ya Olosokwani, ambako alizindua mradi mkubwa wa maji ya visima virefu wilayani Ngorongoro, juzi. Anayeshuhudia ni Mkuu wa  Wilaya ya Ngorongoro,Hashimu Shaibu.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akifurahia jambo na wakazi wa kijiji Olosokwani, baada ya kuzindua mradi wa maji wa visima virefu wilayani Ngorongoro juzi. Kushoto ni Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania, Mbarouk Nassor Mbarouk.

Na Loveness Bernard

Wafugaji kutoka nchi za jirani  waliovamia katika eneo la Loliondo  wametakiwa kuondoa mifugo yao mara moja ili kuliacha eneo hilo kubaki na amani.

Akizungumza na wananchi na wafugaji wa kijiji cha Ololosokwani, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema wakazi wa Loliondo wanauwezo wa kutatua migogoro yao wenyewe ila wanaosababisha migogoro hiyo isiishe na kuibuka mara kwa mara ni wageni wanaoingia katika eneo hilo na kuchungia mifugo yao.

“Ninatoa tahadhali kwa wageni wanaoitazama loliondo kwa jicho la husda waache kufugia mifugo yao loliondo, kila mmoja afugie kwao ardhi ya loliondo ni ya wana loliondo na sio wageni” alisema Nyalandu.

Alisema changamoto kubwa inayoikabili eneo hilo la Loliondo ni ongezeko la watu na mifugo wakati ardhi ikibaki kuwa ile ile.

Nyalandu alisema kuna haja ya kuendeleza uhifadhi ili eneo la Loliondo liendelee kustawi na wageni waendelee kuja Loliondo ambapo watachangia utalii endelevu katika shughuli kama za utalii wa picha na uwindaji.

Akizungumzia kuhusu miradi ya maji aliyoikabidhi kwa wananchi wa loliondo jana kutoka kwa Balozi wa Falme za Kiarabu waliofadhiri ujenzi wa miradi hiyo iliyogharimu sh bilioni 1.6 Waziri Nyalandu alisema hayo ni matunda  ya ushirikiano mzuri baina ya Rais Jakaya Kikwete na Mfalme wa Dubai Shekh Makthum na Jumuiya  ya falme za kiarabu.

Alisema utekelezaji wa miradi hiyo ni ahadi ya Rais Kikwete kwa maeneo ya wafugaji ambapo alisema azma yake ni kuona tatizo la maji katika maeneo ya wafugaji linamazika na kuona mifugo na wafugaji wakinenepa.

Aliwataka wananchi wa Loliondo kuitunza miradi hiyo kwa faida yao na mifugo yao huku wakitumia muda mwingi kwa kazi za maendeleo ya loliondo.
Post a Comment