Wednesday, April 22, 2015

UFAFANUZI WA ZOEZI LA UHAKIKI WA VYAMA VYA KIJAMII NCHINI.


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inapenda kutoa ufafanuzi  kuhusu zoezi linaloendelea kuhusiana na Vyama vya Kijamii vilivyosajiliwa chini ya Sheria ya Vyama, Sura 337 kuwa ni la kubaini vyama vile ambavyo havitekelezi matakwa ya kisheria ya kuwasilisha taarifa za mwaka za ukaguzi wa hesabu za vyama husika na pia vile ambavyo havilipi ada ya mwaka kama sheria ya Vyama inavyoelezea.

 Vyama ambavyo vitabainika kukiuka matakwa ya kisheria kama yaliyotajwa hapo juu ndio vitakavyofutwa kutoka katika Daftari la Msajili wa Vyama vya Kijamii.  Orodha ya Vyama vitakavyofutwa itaanza kutolewa kwa awamu kuanzia wiki hii na kwa kuanzia, orodha hiyo itahusu Vyama vilivyosajiliwa mkoni  Dar es Salaam.
 Kufuatana na orodha tuliyonayo kiasi cha vyama 10,000 vya Kijamii na Taasisi za Dini vimesajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na vitakavyofutwa ni vile tu ambavyo haviwasilishi taarifa za kila mwaka za ukaguzi wa hesabu zao na pia kama havilipi ada ya kila mwaka kama sheria inavyotaka.  Hii ina maana kuwa vile ambavyo vinatekeleza matakwa hayo ya kisheria havitafutwa.
Kwa taarifa hii napenda kueleza kuwa sio Vyama vyote vya Kijamii na Taasisi za Dini vitakavyofutwa na wala hakuna mpango wa kuanza upya zoezi la Usajili wa Vyama vya Kijamii.  
Aidha ni vyema ikaeleweka kuwa zoezi linaloendelea kwa sasa halihusiani na Taasisi zinazoelezewa kujiingiza katika masuala ya kisiasa na pia ieleweke kuwa Wizara yetu haihusiki na usajili wa NGO.


Imetolewa na Isaac J. Nantanga 
MSEMAJI WA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI 

No comments: