Wednesday, April 1, 2015

BUNGE LAPITISHA SHERIA YA KUANZISHWA BARAZA LA VIJANA.


Na Anitha Jonas – MAELEZO,Dodoma.

Serikali inatarajia kuanzisha Baraza la Vijana litakalo kuwa chombo cha vijana kitakacho waunganisha Kitaifa bila kujali itikadi zao za Kisiasa,Imani zao za Kidini wala tofauti zao za Rangi,hayo yamesemwa na Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Mhe.Fenella Mukangara alipokuwa akisoma Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana Tanzania Bungeni Mjini Dodoma.

Mheshimiwa Mukangara aliendelea kusema Baraza hilo litaisaidia Serikali kuweza kuwafikia vijana kwa urahisi na kusikiliza shida zao pamoja na kutoa ufumbuzi wa hoja mbalimbali za vijana.Hata hivyo chimbuko la Muswada huo ni katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya 2007,Ibara ya 3 Sehemu ndogo ya 11 inayosema kwa uwazi Serikali itawezesha kuundwa kwa Baraza Baraza la Vijana na kuanzisha mfumo wa kisheria ili kuliwezesha kufanya kazi.

“Madhumuni ya Muswada huu ni Kutunga Sheria ya Baraza la Vijana Tanzania(The Youth Council of Tanzania 2015) ili kuwa na chombo cha Kitaifa cha kuwewezesha vijana kujadili masuala yao,kutambua majukumu yao,kukuza maadili mema,kukuza moyo wa umoja ,uzalendo,uwajibikaji na kujitolea kwa malengo chanya miongoni mwao katika nchi yetu,”alisema Mhe.Mukangara.

Mbali na hayo katika sehemu ya pili kifungu cha 4-15 cha Muswada huo unaeleza juu ya masharti mbalimbali kuhusu Uanzishwaji,Uanachama,Muundo na kazi za Baraza.Pia sehemu hii imefafanua Mamlaka ya Baraza na vyombo vya utendaji katika ngazi ya Taifa,Mkoa na Wilaya.

Aidha,kwa upande wa maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii yaliyosomwa na Mwenyekiti wake Said Mtanda aliishauri Serikali katika kifungu cha 4(3)Kisomeke Uanachama utakuwa na uwazi na hiari kwa kijana yeyote mwenye umri wa kuanzia miaka 15 mpaka 35.Pia kifungu cha 4(4) imeeleza kuwa baraza halitakuwa kisiasa liongezwe neno halitakuwa na Itikadi za Kidini.

Katika kipindi cha majadiliao ya Muswada huo naye Mhe.Kuluthum Mchuchuri (Mb) Viti Maalum CUF aliipongeza Serikali kwa mchakato wake mzuri wa kuandaa Baraza la Vijana litakalo saidia vijana kujadili matatizo yao na kuyawasilisha Serikali kwa kupatiwa ufumbuzi kwa urahisi,pia ameishauri Serikali katika suala la wajumbe uwawakilishi waanze kuanzia ngazi ya Kata na Serikali pia iweke wazi ni kwa utaratibu gani wawakilishi hao watapatikana.

Naye Mhe.Magret Sitta Mbunge wa Viti Maalum CCM aliiomba Serikali kuandaa ziara kwenda kuangalia mabaraza ya Vijana katika nchi za wenzetu yanafanyaje kazi na kujifunza,pia aliendelea kuiomba Serikali itoe mafunzo mbalimbali ya ufundi kwa kushirikia na taasisi ya Veta na Vyuo vya Wananchi ilikuwapatia elimu itakayo wasaidia vijana kujikwamua kiuchumi na kupunguza idadi ya vijana wa vijiweni.

Pamoja na hayo naye Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR) Mhe.Moses Machali alishauri Serikali Kuanzisha asasi moja ambayo vijana watakayo jiunga huko ili kudhibiti uanzishwaji wa asasi bandia kwa watu wenye nia ya kujinufaisha,pia aliipongeza Serikali kwa kuleta Muswada huo kwani unamanufaa Makubwa kwa vijana.

Aidha,mbali ya kuwepo na marekebisho mbalimbali ya Muswada huo Serikali iliyapokea maombi ya Suala la Baraza hilo kuanzia katika ngazi ya Kata ilikupata uwakilishi uliyowa uhakika na baraza likalete manufaa kwa kuanzia ngazi ya chini ambapo ndipo vijana wengi wanapatikana na jamii inawafahamu kwa usahihi zaidi.

Halikadhalika Serikali iliridhia kuanzishwa kwa uwakilishi wa vijana watano kutoka kundi maalum kwa maana ya wenye ulemavu na ili kuweka uwianao wa vijana hawa kuweza kuwasilisha maombi yao kwa Serikali kwa urahisi huku ikizingatia mahitaji yao maalum.

No comments: