Saturday, February 21, 2015

TAARIFA KWA UMMA.




UAMUZI WA BODI YA WAKURUGENZI KUHUSU MAOMBI YA TPDC YA  TOZO ZA HUDUMA ZA KUCHAKATA NA KUSAFIRISHA GESI ASILIA

1.                  Tarehe 1 Septemba 2014, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilipokea ombi Na. TR-G-14-039 kutoka kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhusu kanuni ya kukokotoa tozo za huduma ya kuchakata na kusafirisha Gesi Asilia, na mapendekezo ya bei ya uchakataji na usafirishaji wa gesi asilia.
2.                  Kati ya Septemba 2014 na Januari 2015, EWURA ilifanya uchambuzi wa kupitia gharama za ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia, muundo wa mtaji (capital structure)  na  faida ya mtaji, gharama za uendeshaji wa mradi, pamoja na tozo iliyoombwa na TPDC.  
3.                  Kwa mujibu wa ombi husika, TPDC waliiomba EWURA kuidhinisha vipengele vifuatavyo:
(a)      kanuni ya kurekebisha tozo za kuchakata na kusafirisha gesi asilia itumike kwa miaka 20 hadi mwaka 2034;
(b)     tozo kwa huduma ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia iwe Dola za Marekani 4.178 kwa uniti (MMBtu) kwa muda wa miaka mitatu ya kwanza;
(c)      faida kwenye mtaji ya asilimia kumi na nane (18%) na muundo wa mtaji wa asilimia hamsini mkopo na asilimia hamsini fedha za TPDC (50:50); na
(d)     mwezi Septemba kila mwaka wa tatu utakuwa ni mwezi ambao marekebisho ya tozo kwa miaka mitatu inayofuata yatawasilishwa kwa EWURA.
4.                  Kwa mujibu wa kifungu 19(2)(b) cha Sheria ya EWURA (Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania), tarehe 27 Novemba 2014, EWURA ilianza mchakato wa taftishi kukusanya maoni na hoja za wadau kuhusu uhalali wa ombi lililowasilishwa na TPDC. Wadau waliowasilisha maoni na hoja mbalimbali ni Baraza la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (CCC), Baraza la Ushauri la Serikali kuhusu Huduma za Nishati na Maji (GCC), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Kampuni ya Saruji Tanzania (TPCC), PanAfrican Energy Tanzania Limited, Songas Limited, Maurel & Prom, Wizara ya Fedha, Wizara ya Maji, na Wizara ya Nishati na Madini. Aidha, hoja za wadau na ufafanuzi uliotolewa na TPDC vimezingatiwa na EWURA katika kutoa uamuzi wa ombi hilo.
5.                  Tarehe  8 Januari na 6 Februari 2015, EWURA ilifanya mikutano na wadau wa karibu (Exit Conference) ambapo EWURA ilisambaza rasimu ya Agizo la EWURA (Draft Order) ili ijadiliwe na kupata maoni ya mwisho; na mkutano huo ulihudhuriwa na  wawakilishi wa Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Maji, Wizara ya Fedha, CCC, GCC, TANESCO, TPDC, PAT, Songas, na TPCC. Asasi zote hizo zilitoa maoni ya mwisho kwenye rasimu ya Agizo la EWURA. Kwa ujumla, EWURA imezingatia maoni yaliyopatikana katika mikutano hiyo na hatimaye kufikia maamuzi kwenye Ombi la TPDC.
6.                  Katika kikao chake cha tarehe 19 Februari 2015, Bodi ya Wakurugenzi ya EWURA, ilijadili Ombi la TPDC na kufikia maamuzi ya kipindi kifupi cha miezi mitatu (Interim Tariff) ambacho TPDC itakitumia kukamilisha ujenzi na kuwasilisha gharama halisi ambayo EWURA iliyahoji. Maamuzi yaliyotolewa ni kama ifuatavyo:




(a)              kanuni ya kukokotoa tozo za kuchakata na kusafirisha gesi asilia iliyoombwa ilirekebishwa na kupitishwa ili itumike kwa miaka 20 kuanzia mwezi Aprili 2015, na kurekebishwa kila baada ya miaka mitano;

(b)              gharama za Mradi wa Bomba la kusafirisha gesi asili kutoka  Mtwara-Dar es Salaam zilizopitishwa ni sawa na Dola za Marekani 1,331.51 milioni, ambapo gharama hizi zitabaki hivyo hadi mwezi Juni 2015 ambapo gharama halisi za mradi zitakapojulikana na kufungwa;
(c)              gharama za uendeshaji zitakuwa sawa na Dola za Marekani 241.58 milioni kwa mwaka;



(f)               tozo ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia italipwa kwa Shilingi za Tanzania, kwa kiasi sawa na jumla ya Dola za Marekani 2.14 kwa uniti, ambapo tozo ya kuchakata gesi asilia itakuwa Dola za Marekani 0.95 kwa uniti. Kati ya hizo, na tozo la kusafirisha gesi asilia itakuwa Dola za Marekani 1.19 kwa uniti. Tozo hizi zitatumika hadi hapo EWURA itakapotoa agizo lingine baada ya kutathmini gharama halisi za mradi zitakapojulikana na ujenzi kukamilika;
(g)              endapo EWURA haitatoa agizo jingine, tozo za kuchakata na kusafirisha gesi asilia kama zinavyoonekana kwenye aya ya 6(f) hapo juu zitaendelea kwa miaka mitatu (Aprili 2015 hadi Juni 2018);
(h)              faida kwenye mtaji ya asilimia 4.58 na uwiano wa mtaji wa asilimia 75 fedha za mkopo na asilimia 25 fedha za TPDC (75:25); na
(i)                mwezi Septemba kila mwaka wa tatu, utakuwa ni mwezi ambao marekebisho ya tozo kwa miaka mitatu inayofuata yatawasilishwa kwa EWURA.

7.                  Pamoja na maamuzi hayo hapo juu, TPDC wanaagizwa kutekeleza masharti yafuatayo:-

(a)             kuzingatia kanuni za ushindani kama zilivyoainishwa katika Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2011 (Public Procurement Act, 2011) na kuiarifu EWURA kila TPDC inapofanya manunuzi ya thamani yanayozidi dola za Marekani 5 milioni.
(b)            endapo kuna ulazima wa kutumia utaratibu  wingine kwa mujibu wa Sheria, ndani ya siku thelathini (30) baada ya kuingia mikataba ya manunuzi TPDC italazimika kutoa taarifa na kuwasilisha nakala za mikataba EWURA;

(c)             ndani ya kipindi cha miezi kumi na miwili (12) baada ya Agizo la EWURA, kuwasilisha EWURA, mpango wa uendelezaji wa miundombinu ya gesi asilia (the Natural Gas Infrastructure Development Plan);
(d)            ndani ya kipindi cha miezi kumi na miwili (12) baada ya Agizo la EWURA,  kuwasilisha EWURA, mpango wa utumiaji wa miundombinu ya gesi asilia iliyojengwa (the Natural Gas Infrastructure Utilisation Plan);

(e)             ndani ya kipindi cha miezi kumi na miwili (12) tokea kuanza kwa Agizo la EWURA, kuandaa Mkataba wa Huduma kwa Wateja, ili kupima ufanisi katika kutoa huduma za usambazaji wa gesi asilia na kushughulikia malalamiko ya wateja.
(f)             kuhakikisha kwamba mfuko wa dhamana kwa ajili ya manunuzi ya gesi kutoka kwa wawekezaji wenye visima vya gesi asilia unakuwa wa kiasi cha fedha kisichopungua Shilingi 153 bilioni kila wakati kwa kipindi chote cha mradi; Aidha;
(g)            Kabla ya kuanza kutumika kwa Mkataba wa Huduma kwa Wateja, kuwasilisha mkataba huo EWURA kwa ajili ya kuupitisha; na

Agizo hili  litaanza kutekelezwa kuanzia tarehe 1 APRILI  2015

 


 

IMETOLEWA NA

FELIX NGAMLAGOSI

MKURUGENZI MKUU
20 FEBRUARI 2015

No comments: